MANISPAA YAFIKIA ASILIMIA 93 UJENZI WA KITUO CHA AFYA LIKOMBE - MTWARA MIKINDANI MANISPAA

Jumatano, 3 Januari 2018

MANISPAA YAFIKIA ASILIMIA 93 UJENZI WA KITUO CHA AFYA LIKOMBEJengo la nyumba ya mganga

Na Jamadi Omari

 Manispaa ya Mtwara-Mikindani Hadi kufikia Disemba 31,2017 imefikisha asilimia 93 ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika kituo cha afya likombe  na kugharimu kiasi cha fedha shilingi milioni  326,457,759.18 kati ya milioni 500 zilizotolewa na Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.
Asilimia 7 iliyobaki inatarajia kukamilika baada ya wiki mbili kuanzia Januari 1,2018 na kwamba hadi kukamalika kwa mradi huo Manispaa imekadiria kutumia milioni 400 na kubakiwa na shlingi milioni 100 zitakazotumika  katika ujenzi  na ukamilishaji wa miundombinu mingine katika kituo hiko ikiwemo ukarabati wa jengo La OPD , Ujenzi wa choo cha wagonjwa wanaokuja kutibiwa kwenye kituo hicho ambacho kitagharimu Shilingi milioni 15.
Akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo iliyofanyika Januari 1,2018 kati ya Timu ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara na Timu ya Menejiment ya halmashauri Mkurugenzi wa Manispaa Bi Beatrice R. Dominic amesema kuwa Ujenzi wa mradi wa miundombinu ya afya  unaendelea vizuri na kwa gharama inayoridisha.
Akielezea kuhusu mikakati iliyotumika katika ujenzi huo hadi kupelekea kukisia kubakiwa na fedha zilizotajwa Beatrice amesema kuwa Ofisi yake imetii  agizo la Serikali lililotaka mradi huo kujengwa kwa kutumia mafundi wenyeji  ambao wametoa gharama za ujenzi zilizo halisi na kazi imekuwa nzuri,na kwamba kila jengo amepewa fundi mmoja  na vibarua wake.
Ameongeza kuwa Menejimenti ya halmashauri ilikubaliana vifaa vyote vya ujenzi vinunuliwe viwandani ikiwemo mabati,Gypsum,Tiles,rangi,cable za umeme na vifaa vingine  ili kuweza kupunguza gharama na vifaa vichache vilinunuliwa kwenye eneo la Manispaa pamoja na mafundi waliojenga majengo hayo.

Aidha amesema kuwa mradi umefikia hapo kwa kuwa kulikuwa na umakini mkubwa kwenye usimamizi na kwenye kufanya makadirio  Lakini pia ushirikiano ulikuwa mkubwa kati ya timu ya halmashauri na Timu ya uendeshaji wa kituo.

Nae Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara Duncan Thebas amepongeza Manispaa kwa kazi nzuri iliyofanyika na kwamba inadhihirisha maamuzi sahihi ya Serikali ya kuikomboa Tanzania kwa kutumia mafundi wenyeji kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo. Aidha amepongeza ujenzi wa njia za kupita(walk way) ambayo kwenye maelekezo ya mradi haikuwepo lakini Manispaa imeona umuhimu wa kujenga .


 

 Jengo la wodi ya Mama na Mtoto


Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa DR.Christa Nzali ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha hizo kwani kukamilika kwa majengo hayo kutasaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kupunguza vifo vya akina mama na watoto, kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Mkoa.

Wakati huo huo Fundi aliyepewa kazi ya ujenzi wa Wodi ya  Mama na Mtoto Athumani Bandiko ameishukuru Serikali kwa kuwapatia kazi ya ujenzi kwani imewapa nafasi ya wao kuonesha uwezo wao kama mafundi wadogo lakini pia imesaidia kutengeneza ajira kwa vijana. AIdha ameiomba Serikali iwaamini na iendelee kuwapa kazi katika majengo mengine.

 Manispaa Mtwara-Mikindani Oktoba 13,2017 ilipokea fedha kiasi cha shilingi 500 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika Kituo cha afya Likombe, Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na Wodi ya Mama na Mtoto, Maabara, Chumba cha kulaza Maiti, Chumba cha Kufulia nguo, Kichomea taka pamoja na ujenzi wa Nyumba ya Mganga.

 

 Timu ya Ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Timu ya Menejiment wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kumaliza ukaguzi

Hakuna maoni:

Copyright: mtwaramikindanimc©2018