MTWARA-MIKINDANI YATUMIA SHILINGI MIL 834.1 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO - MTWARA MIKINDANI MANISPAA

Jumanne, 16 Januari 2018

MTWARA-MIKINDANI YATUMIA SHILINGI MIL 834.1 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO




Muonekano wa ndani wa jengo la machinjio ya Chuno baada ya kufanyiwa ukarabati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani

Na Jamadi Omari


Katika kuhakikisha kuwa Manispaa Mtwara-Mikindani inaendelea kuboresha huduma za Jamii kwa Wananchi wake, imetoa na kutumia fedha kiasi cha shilingi milioni  834,074,361.79 kutoka katika mapato yake ya ndani Kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo, kuchangia mfuko wa Wanawake na Vijana pamoja na ulipaji fidia kwa wananchi.

Akizungumza Ofisini kwake mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Bi Betarice Dominic amesema kuwa fedha ni mapato yatokanayo na kodi mbalimbali zinazolipwa na Wananchi na hivyo Manispaa imeona umuhimu wa kuzirudisha kwao ili kuimarisha miundombinu mbalimbali inayowagusa moja kwa moja.

Amesema kuwa Miradi iliyopelekewa fedha imegusa sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya elimu, Utawala, Ufugaji na Uvuvi,Barabara,Afya pamoja na Kilimo. Aidha amewashukuru na kuwapongeza Wananchi  wa manispaa kwa kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi na kuwataka kuwa na utamaduni huo ili kuijenga Manispaa iliyo bora na yenye kuonekana.




 Jengo la mwalo wa Mikindani lililopo Kata ya jangwani likiwa kwenye hatua ya umaliziaji
 
Kwa upande wake Afisa Mipango wa Manispaa Ernest Mwongi amesema kuwa fedha zote zilizotolewa zimeshapelekwa kwenye Akaunti za miradi husika na kuna miradi mingine imeshatekelezwa na kukamilika, na miradi mingine  ipo kwenye hatua ya utekelezaji na kwamba  idara  ya mipango inahakikisha inaifuatilia kwa ukaribu miradi iliyobaki ili iweze kukamilika kwa wakati.

Ameitaja Miradi inayotekelezwa kulingana na fedha iliyotolewa ni pamoja na Mradi wa ujenzi  wa zahanati Mbawala chini, UKarabati wa Machinjio, Ujenzi wa matundu ya vyoo Shule ya Msingi Mbae na Mtawanya, Ujenzi wa Vyoo Shule za  Msingi Mjimwema, Shangani na Mlimani.

Miradi mingine ni Ujenzi wa Kalvati Miseti, Ununuzi wa pikipiki 5 kwa ajili ya watendaji wa Kata, Ununuzi wa gari la Mkurugenzi, Ujenzi wa Uzio  Ofisi kuu ya Manispaa, Ujenzi wa Shedi mwalo wa samaki Mirumba, Ununuzi wa gari la kufagia barabara pamoja na Ujenzi wa nyumba  za Wakuu wa Idara.

 Fedha hizo vilevile zimeelekezwa katika Ujenzi wa Ofisi ya Kata Mtawanya na Tandika, Umaliziaji wa ujenzi Ofisi ya Kata Jangwani, Ujenzi wa choo soko la kiyangu, Ujenzi wa nyumba za walimu Namayanga, Ujenzi wa soko la Mitengo, Uandaaji na ununuzi wa miche ya Korosho, Ununuzi wa mbegu za Mtama, uwekaji wa nguzo na minyororo barabara ya TANU, Ujenzi wa vyumba vya madarasa 3 Shule ya Sekondari Mitengo na Mangamba, Pia Utengenezaji wa madawati na uwekaji wa Taa Stendi kuu ya mabasi.



 Sehemu ya uzio wa jengo la ofisi kuu,ujenzi huo unaendelea

Asha Mapesa mkazi wa Chuno amepongeza Manispaa kwa kazi wanayoifanya ya kuleta maendeleo na kuahidi kutoa ushirikiano kwenye kulinda rasilimali hizo kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

Baada ya kufanya Mapitio ya bajeti 2017/2018 mwezi Desemba 2017, Manispaa Mtwara-Mikindani imepanga kukusanya bilioni 4,601,204,136 kutoka katika mapato yake ya ndani, Hadi Desemba 31,2017 Manispaa imekusanya bilioni 2,720,578,528 sawa na asilimia 59 ya bajeti iliyopangwa.

 Ujenzi wa matundu ya vyoo Shule ya Msingi Mtawanya ukiwa kwenye hatua za umaliziaji

Hakuna maoni:

Copyright: mtwaramikindanimc©2018