Januari 16, 2018
BY Mtwara Mikindani Manispaa0
Comments
Muonekano wa ndani wa jengo la machinjio ya Chuno baada ya kufanyiwa ukarabati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani
Na Jamadi Omari
Katika kuhakikisha
kuwa Manispaa Mtwara-Mikindani inaendelea kuboresha huduma za Jamii kwa
Wananchi wake, imetoa na kutumia fedha kiasi cha shilingi milioni 834,074,361.79 kutoka
katika mapato yake ya ndani Kutekeleza miradi mbalimbali
ya Maendeleo, kuchangia mfuko wa Wanawake na Vijana pamoja na ulipaji fidia kwa
wananchi.
Akizungumza Ofisini
kwake mkurugenzi wa Manispaa Mtwara-Mikindani Bi Betarice Dominic amesema kuwa fedha
ni mapato yatokanayo na kodi mbalimbali zinazolipwa na Wananchi na hivyo Manispaa
imeona umuhimu wa kuzirudisha kwao ili kuimarisha miundombinu mbalimbali
inayowagusa moja kwa moja.
Amesema kuwa Miradi
iliyopelekewa fedha imegusa sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya elimu, Utawala,
Ufugaji na Uvuvi,Barabara,Afya pamoja na Kilimo. Aidha amewashukuru na kuwapongeza
Wananchi wa manispaa kwa kutekeleza wajibu
wao wa kulipa kodi na kuwataka kuwa na utamaduni huo ili kuijenga Manispaa
iliyo bora na yenye kuonekana.
Jengo la mwalo wa Mikindani lililopo Kata ya jangwani likiwa kwenye hatua ya umaliziaji
Kwa upande wake Afisa
Mipango wa Manispaa Ernest Mwongi amesema kuwa fedha zote zilizotolewa zimeshapelekwa
kwenye Akaunti za miradi husika na kuna miradi mingine imeshatekelezwa na kukamilika,
na miradi mingine ipo kwenye hatua ya utekelezaji
na kwamba idara ya mipango inahakikisha inaifuatilia kwa
ukaribu miradi iliyobaki ili iweze kukamilika kwa wakati.
Ameitaja Miradi
inayotekelezwa kulingana na fedha iliyotolewa ni pamoja na Mradi wa ujenzi wa zahanati Mbawala chini, UKarabati wa
Machinjio, Ujenzi wa matundu ya vyoo Shule ya Msingi Mbae na Mtawanya, Ujenzi
wa Vyoo Shule za Msingi Mjimwema,
Shangani na Mlimani.
Miradi mingine ni Ujenzi
wa Kalvati Miseti, Ununuzi wa pikipiki 5 kwa ajili ya watendaji wa Kata,
Ununuzi wa gari la Mkurugenzi, Ujenzi wa Uzio Ofisi kuu ya Manispaa, Ujenzi wa Shedi mwalo
wa samaki Mirumba, Ununuzi wa gari la kufagia barabara pamoja na Ujenzi wa
nyumba za Wakuu wa Idara.
Fedha hizo vilevile zimeelekezwa katika Ujenzi
wa Ofisi ya Kata Mtawanya na Tandika, Umaliziaji wa ujenzi Ofisi ya Kata
Jangwani, Ujenzi wa choo soko la kiyangu, Ujenzi wa nyumba za walimu Namayanga,
Ujenzi wa soko la Mitengo, Uandaaji na ununuzi wa miche ya Korosho, Ununuzi wa
mbegu za Mtama, uwekaji wa nguzo na minyororo barabara ya TANU, Ujenzi wa vyumba
vya madarasa 3 Shule ya Sekondari Mitengo na Mangamba, Pia Utengenezaji wa
madawati na uwekaji wa Taa Stendi kuu ya mabasi.
Sehemu ya uzio wa jengo la ofisi kuu,ujenzi huo unaendelea
Asha Mapesa mkazi wa
Chuno amepongeza Manispaa kwa kazi wanayoifanya ya kuleta maendeleo na kuahidi
kutoa ushirikiano kwenye kulinda rasilimali hizo kwa manufaa yao na vizazi
vijavyo.
Baada ya kufanya
Mapitio ya bajeti 2017/2018 mwezi Desemba 2017, Manispaa Mtwara-Mikindani
imepanga kukusanya bilioni 4,601,204,136 kutoka katika mapato yake ya ndani,
Hadi Desemba 31,2017 Manispaa imekusanya bilioni 2,720,578,528 sawa na asilimia
59 ya bajeti iliyopangwa.
Ujenzi wa matundu ya vyoo Shule ya Msingi Mtawanya ukiwa kwenye hatua za umaliziaji